Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah al-Udhma Sheikh Bashir Najafi, mmoja wa Maraji' wa taqlid wa Najaf Ashraf, leo Alhamisi katika taarifa yake ametoa salamu za rambirambi kufuatia kufariki kwa Marji' mkubwa wa kidini, Ayatullah al-Udhma Sheikh Muhammad Is’haq Fayyadh.
Ayatullah Sheikh Bashir Najafi katika taarifa yake ya rambirambi amesema: “Katika mojawapo ya siku kuu kabisa za Mwenyezi Mungu Mtukufu, tukiwa na nyoyo zenye subira na zenye kuiamini ahadi ya Mwenyezi Mungu, tunatoa salamu za pole kwa kufuatia kuondoka kwa mmoja wa wakubwa katika jamii na mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Uislamu, Marjii mkubwa wa kidini, Ayatullah al-Udhma Sheikh Muhammad Is’haq Fayyadh.”
Aliongeza kwa kusema: “Katika msiba huu mkubwa uliosababisha pengo katika mwili wa Uislamu, tunatoa salamu za rambirambi kwa Hujja wa Mwenyezi Mungu, Imam Hujjat ibn al-Hasan (roho zetu ziwe fidia kwake), kwa wanazuoni wa Kiislamu, Hawza za kielimu, familia tukufu ya marehemu na waumini wote.”
Ayatullah Najafi aliendelea kusema: “Mwenyezi Mungu amrehemu; alikuwa kwetu kaka mkubwa, mwenye huruma na mlinzi wa Hawza tukufu ya kielimu, ambaye alikuwa akijitolea kwa ajili ya kuihifadhi na kuilinda, Marjii huyu marehemu alinufaika na elimu za Kimungu na akazama katika kina chake mpaka yeye mwenyewe akawa chemchemi kwa wengine, alikuwa na uhusiano wa karibu na wakubwa na wanazuoni wetu — Mwenyezi Mungu awarehemu — kiasi kwamba wakati wa kupoteza kwao, alikuwa sababu ya faraja kwetu.”
Mwisho wa taarifa yake alisema: “Leo mzee na Sheikh wa Najaf Ashraf ametutoka ili akafanye upya ahadi yake katika birika ya Kawthar pamoja na Wilayah ya Amirul-Mu’minin Ali (as).
فَإِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ، وَلَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّهِ الْعَلِيِّ الْعَظِيمِ
Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake Yeye tutarejea; wala hakuna nguvu wala uwezo isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliye juu na Mkuu.”
Maoni yako